Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imetangaza kushuka kwa bei ya Petroli na Dizeli kwa asilimia 2.7 (shilingi 61) na asilimia 3.8 (Shilingi 88) na ongezeko la asilimia 0.09 (shilingi 2) kwa mafuta ya taa.
Hayo yamebainishwa na taarifa zilizotolewa na mamlaka hiyo na kusisitiza kuwa bei hizo zitaanza kutumika rasmi leo Mei 02, 2018 kwa nchi nzima.
Aidha, EWURA imesema kubadilika kwa bei hizo kumetokana na kushuka kwa bei za mafuta katika soko la dunia na kupungua kwa gharama za usafirishaji wa mafuta (BPS Premium) pamoja na kuchangiwa kwa kubadilika kwa kanuni ya kukokotoa bei za mafuta nchini ili kujumuisha gharama kwa wakala wa serikali na tozo za huduma za Manispaa na Jiji kwa wauzaji wa mafuta kwa jumla na rejareja.
Pamoja na hayo, taarifa hiyo imeendelea kwa kusema “ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja. Adhabu kali itatolewa kwa kituo husika kwa kutotekeleza matakwa ya kisheria kwa mujibu wa kanuni husika”.
Kwa upande mwingine, EWURA imewataka wauzaji wa mafuta ya petroli kutoa risiti za mauzo kutoka kwenye mashine za EFPP (Electronic Fiscal Pump Printers) huku wanunuzi wakiombwa kuhakisha wanapata stakabadhi hizo za malipo zinazoonyesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita.