Rais wa Marekani, Donald Trump ametishia kuifunga serikali kuu mwaka huu endapo bunge la nchi hiyo halitaidhinisha bajeti ya kutosha kwa ajili ya usalama mipakani, ikijumuisha fedha za kujenga ukuta kati ya mpaka wa Marekani na Mexico.
Mwezi uliopita, Rais Trump alitia saini mswaada wa sheria wa matumizi ya dola trilioni 1.3 ambazo zinaendelea kuendesha shughuli za serikali kuu hadi mwisho wa mwezi Septemba mwaka huu.
Aidha, Trump amesema kuwa bunge linatazamiwa kupigia kura mswaada wa sheria wa bajeti ya matumizi ya mwaka ujao Septemba 28, lakini kama haitajumuisha fedha kwa ajili ya ukuta, yeye hatatia saini mswaada huo.
Hata hivyo, wakati wa Kampeni, Trump alitoa ahadi ya kujenga ukuta kati ya Marekani na Mexico ili kuweza kudhibiti wahamiaji na wafanyabiashara wa dawa za kulevya.