Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ifikapo Mei 15 inatarajia kutoa uamuzi wa kesi ya kufanya maandamano na mkusanyiko usio halali inayowakabili viongozi 9 wa CHADEMA akiwemo Freeman Mbowe kama iende Mahakama Kuu ama laa.
Hatua hiyo inatokana na mvutano wa hoja za kisheria zilizotolewa jana na Wakili wa utetezi, Peter Kibatala kisha kujibiwa leo na Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri.
Katika majibu yake Wakili Nchimbi ameiomba mahakama hiyo kutupilia mbali hoja za utetezi zilizotolewa na Kibatala kwa sababu zitapelekea ucheleweshaji wa shauri hilo pasipokuwa na sababu za msingi.
Nchimbi amedai kuwa katika mazingira ya mwenendo wa kesi hiyo toka ilipoanza hadi leo hakuna swali lolote la msingi lililoibuliwa na upande wa utetezi ambalo linajikita na uvunjifu ama ukiukwaji wa haki ya kikatiba.
Alibainisha kuwa ukiangalia mlolongo wa hati ya mashtaka ni hati ambayo washtakiwa wamesomewa mashtaka zaidi ya mara moja ama mbili ikiwamo jana na washtakiwa waliyasikia mashtaka, wakayaelewa ndiyo maana wakaenda mbele wakayakanusha.
Nchimbi amedai kuwa washtakiwa wamefunguliwa kesi ya jinai wakati walikuwa katika mkutano halali wa kampeni ya uchaguzi mdogo na kwamba kuwafungulia mashtaka hayo ni uvunjifu wa haki ya kikatiba, alisisitiza kuwa ni rai ya upande wa mashtaka kwamba yote yaliyoongelewa na upande wa utetezi hayawezi kuitwa ni maswali ya kikatiba ambayo yangeilazimu mahakama kupeleka kesi hiyo Mahakama Kuu.
Baada ya kutolewa kwa hoja hizo,Wakili Kibatala aliiaambia mahakama kuwa mchakato wa kijinai ni mchakato mtakatifu ambao haukukusudiwa kuwashtaki watu ambao wanatekeleza majukumu yao kikatiba.