Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ameelezea wasiwasi wake kwa wanachama watano wa kudumu wa Baraza la Usalama kuhusu mgogoro wa Syria, akisisitiza haja ya kuiepusha hali hiyo kuzidi kiwango cha kudhibitiwa.
Kauli za Guterres zimefuatia hatua ya baraza hilo kushindwa kukubaliana kuhusu jibu la shambulizi linalodaiwa kuwa la sumu ambalo lilifanywa mwishoni mwa wiki katika mji wa Douma unaodhibitiwa na waasi nchini Syria na kuzusha hasira kote duniani.
Wakati huo huo, Urusi na Iran zimemshambulia Rais wa Marekani Donald Trump baada ya rais huyo kusema kuwa Marekani itafanya mashambulizi ya makombora dhidi ya serikali ya Syria kama jibu la shambulizi linalodaiwa kuwa la silaha za sumu.
Urusi imesema inalifuatilia kwa karibu jeshi la wanamaji wa Marekani ambalo liko njiani kuelekea baharani katika ukanda wa pwani ya magharibi mwa Syria.
Afisa mmoja mwandamizi wa Iran, ambayo pia inamuunga mkono Rais wa Syria Bashar al-Assad, amesema nchi yake itamlinda mshirika wake dhidi ya kile alichokiita kuwa ni “uchokozi wa kigeni”