Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda aameweka hadharani kuwa kati ya wanawake 480 waliozungumza na wanasheria siku ya jana Jumatatu katika ofisi za mkoa wamezalishwa na kutelekezwa na wabunge pamoja na viongozi wa dini.
Makonda ametoa kauli hiyo leo mbele ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan wakati wa uzinduzi wa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi kwa wasichana wenye umri wa miaka 14 unaofanyika leo katika viwanja vya Zakeem Mbagala.
Makonda amesema wanawake 47 wanadai wabunge ndio wamewatelekeza na 14 wamesema kuwa wamezalishwa na kutelekezwa na viongozi wa dini.
Pia amesema kuwa “Katika Mkoa wa Dar es Salaam, mwaka 2017 wanawake waliojifungua walikuwa 129,347 na kati ya hao asilimia 60 walitelekezwa na watoto 274 waliokotwa maeneo mbalimbali ndiyo maana tumeona tuje na mkakati huu kuhakikisha tunapambana na wale wanaume wote wanaotelekeza watoto,”.
Mkoa wa Dar es salaam upo kwenye zoezi la kuwapa msaada wa kisheria wanawake wa mkoa huo ambao wametelekezwa na wenzi wao na wale waliokataa kulea watoto wao.