Dk. Mwele Macelela ameteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kanda ya Afrika na kwa hiyo atakuwa mtu wa pili kimamlaka katika Makao Makuu ya Shirika hilo barani Afrika kwa ujumla. Hiyo ina maana kuwa nchi zote za Afrika zitamkimbilia ili kupata mabilioni ya fedha yanayotolewa na WHO kusaidia kuhuisha sekta ya afya.
Mwaka 2016 Uteuzi wa Dk. Mwele Malecela kama Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (National Institute for Medical Research – NIMR) ulitenguliwa na Rais John Magufuli, siku moja baada ya Dk. Mwele kusoma hadharani ripoti iliyoonesha kuwa kuna kina mama wamekutwa na dalili za virusi vya ZIKA nchini Tanzania.
Pamoja na yote hayo, Dk. Malecela anashikilia rekodi nyingi na kubwa sana. Kwa mfano, Dk. Mwele ndiye mwanamke wa kwanza duniani na mwafrika wa kwanza kuteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Kimataifa cha Taasisi za Afya Jamii (IANPHI) taasisi ambayo ni mwamvuli wa taasisi zote za kitaifa za afya kwenye mataifa yote duniani.
Dk. Malecela alijiunga NIMR mwaka 1987 baada ya kuhitimu shahada zake kutoka Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam (UDSM), pia ana Shahada ya Uzamivu (PhD) kutoka Chuo Kikuu cha London Uingereza mwaka 1995.
Sekta ya Afya nchini Tanzania haitamsahau kwa mchango wake mkubwa kwenye kujenga misingi ya tafiti za afya na hasa usimamizi wake kwenye Mchakato wa Kuweka Vipaumbele vya Kitaifa vya Tafiti za Afya ambao ulianzishwa mwaka 1999 na baadaye kufanyiwa mapitio mwaka 2005.