Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM , Humphrey Polepole amefunguka na kuwataka viongozi wa vya vyama vya siasa hasa upinzani wajifunze tabia ya kutokutoa kauli za kihalifu kwa madai wakifanya hivyo watakuwa wametenda kosa kwa mujibu wa sheria za nchi.
Polepole ametoa kauli hiyo asubuhi ya leo (Aprili 09, 2018) kupitia ukurasa wake maalum wa twitter wakati akijibu swali la mmoja wa wananchi ambaye alimtaka Polepole aishauri serikali kuzipuuzia baadhi ya kauli zitolewazo na wapinzani kwa kuziona ni za kisiasa ili kuepusha baadhi ya mambo yanayotokea kwa viongozi wa kisiasa.
“Kauli za kihalifu hazipaswi kupuuzwa, anayetoa kauli za kihalifu anatenda kosa kwa mujibu wa sheria. Kauli za kihalifu ndio hufitinisha watu, huvuruga utangamano, huleta chuki, huzaa ugomvi na migogoro. Viongozi wa upinzani wajifunze kutokutoa kauli za kihalifu”, amesema Polepole.
Aidha, Polepole hakuishia hapo ameendelea kwa kusema “kwa sheria zetu kutusi watu ni kosa, umtukane mtu yeyote ni kosa na nadhani ningekuwa mimi kumtukana mtu ambaye ndiye taswira ya umoja wetu ilipasa kupewa uzito wa ziada kiadhabu. Mazoea ya matusi yanatubomolea maadili yetu kama taifa. Utatukaniwa mama yako halafu unachekacheka”.