Idara ya uhamiaji mkoani Dodoma inawashikilia raia tisa wa kigeni kutoka mataifa mbalimbali wakiwemo wachezaji wanne wa mpira wa miguu kutoka Nigeria.

Afisa uhamiaji katika mkoa huo Peter Kundy amesema raia wanne wa Nigeria waliingia nchini na wakala Gabriel Nkayimbo raia wa Cameroon ili wasajiliwe na klabu ya African Lyon ya jijini Dar es Salaam au Dodoma FC ya Dodoma lakini baada ya kushindwa wakatelekezwa.

Kundy amesema raia hao wametakiwa kuondoka nchini mara moja ambapo raia wengine wanaotoka mataifa ya Burundi, Uganda na Sudan kusini nao wametakiwa kuondoka nchini na kutoa rai kwa mawakala wa wachezaji kufuata utaratibu uliopo wa TFF na FIFA pamoja na wamiliki wa shule, saluni na nyumba za kulala wageni kutowapokea wageni wasiofuata taratibu za nchi.

Mbali na hilo, Jeshi la Polisi mkoa wa Dodoma limewakamata watuhumiwa 23 wa makosa mbalimbali yakiwemo ya wizi wa kuvunja nyumba, uvutaji bangi, mirungi na utapeli baada ya kufanyika msako ndani ya mji huo.

Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, Gilles Muroto akizungumza na waandishi wa habari amesema watuhumiwa hao wamekamatwa wakiwa na mihuri ya mabenki mbalimbali, vitambulisho, nywele za akinamama, bangi, luninga na mirungi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *