Aliyekuwa mke wa Nelson Mandela, Graca Machel, ametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha mwanaharakati wa kupinga ubaguzi wa rangi Afrika Kusini, Winnie Mandela.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Graca alisema Winnie (81) alikuwa mwanamke shupavu wa kupigiwa mfano na ambaye alihamasisha wengi katika kupigania haki na usawa katika jamii.
Amesema kuwa “Maisha yake ya ajabu na kipekee yaliyojaa changamoto na harakati yamekuwa kivutio na hamasa kwa watu wengi katika jamii cha kuonesha jinsi ya kujipa moyo, kutokata tamaa pindi tunapokumbwa na changamoto, huku tukiwa na matumaini ya kwamba tutafanikiwa,”.
Alisema Winnie kwake ni dada mkubwa ambaye amekuwa akipendwa wa watu si wa Afrika Kusini pekee, bali duniani kote kwa ujumla kutokana na upendo wake na kujitoa kupigania ukombozi wa taifa hilo.
Pamoja na kupita katika kipindi hiki cha machungu na huzuni ya kumpoteza mpendwa wao, Graca amewasihi wote walioguswa na msiba huo kujiimarisha na kuendelea kutetea haki za raia katika jamii zinazowazunguka kwani kwa kutenda hivyo watakuwa wakimuenzi Winnie.