Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na viongozi wengine watano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, leo watafika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kwa ajili ya ukamilishaji wa masharti ya dhamana waliyopata mwishoni mwa wiki iliyopita.
Machi 27, Mbowe na wenzake walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na makosa nane, ombi lao la dhamana likaahirishwa uamuzi kwa siku mbili ili Hakimu akajiridhishe.
Alhamisi, Hakimu Wilbard Mashauri alikubali ombi la dhamana licha ya washitakiwa kutokuwepo mahakamani siku hiyo kutokana na gari la kuwatoa mahabusu ya Gereza la Segerea kuharibika.
Mbali na Mbowe (56), washitakiwa wengine ni Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (52), Mbunge wa Kibamba John Mnyika (37), Mbunge wa Musoma Mjini, Esther Matiko (41), Katibu Mkuu, Vincent Mashinji (45) na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu (39).
Hakimu Mashauri alisoma masharti ya dhamana kuwa ni washtakiwa kujidhamini kwa hati ya maneno ya Sh. milioni 20, wadhamini wawili kwa kila mshtakiwa wanaotoka taasisi zinazotambulika watakaosaini hati yenye thamani hiyo ya fedha.