Mkuu wa wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi amewataka watu waliovunja nyumba ya msanii Mandojo kujisalimisha mara moja, kwani ofisi yake haina taarifa juu ya uvunjaji wa nyumba hiyo wala nyinginezo hivi karibuni.
Kwenye ukurasa wake wa instagram Ally Hapi ameandika ujumbe mrefu kuhusu tukio hilo, huku akimpa pole msanii huyo wa muziki wa bongo fleva Man Dojo, na kumtaka afike nyumbani kwake ili aweze kutafuta namna ya kumsaidia.
Kupiatia ukurasa wake Instagram DC, Hapi ameandika “Mchana huu nimeona clip ya msanii Man Dojo ikimuonesha akilalamika kuvunjiwa nyumba yake aliyoijenga kwa jasho lake la muziki na watu asiowajua akiwa safarini.
Watu hao (mabaunsa) wanatajwa kufanya tukio hilo kata ya Mbweni wilayani Kinondoni ingawa video haielezi ni mtaa gani.Ofisi yangu haina taarifa yoyote ya kuvunjwa nyumba eneo la Mbweni. Yeyote mwenye kumfahamu Man Dojo naomba amjulishe kuwa aje anione nyumbani kwangu kesho Jumamosi saa 2 Asubuhi. Na hao waliofanya tukio hilo popote walipo, wajisalimishe kabla sijawatafuta”, ameandika Ally Hapi.
Hivi karibuni watu ambao hawajajulikana walikwenda nyumbani kwa msanii Mandojo huko Mbweni jijini Dar es salaam, na kuvunja nyumba yake ambayo amedai ameijenga kwa hela za muziki, na kuiba baadhi ya vitu na vingine kuviharibu, na alipouliza alisema watu hao walitumwa na OCD wa Kawe, huku akilalamika kuwa hana mgogoro wowote wa ardhi wala hana notice ya kutakiwa kutoka eneo hilo.