Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umesema kuwa uamuzi wa kutengua uteuzi wa Jokate Mwegelo aliyekuwa Kaimu Katibu wa Idara ya Uhamasishaji na Chupukizi unatokana na kukaimu nafasi hiyo kwa mwaka mmoja bila kuthibitishwa.
Kaimu Katibu Mkuu wa umoja huo, Shaka Hamdu Shaka ametoa sababu hizo saa chache baada ya Kamati ya Utendaji kupitisha uamuzi huo dhidi ya Jokate.
Aliongeza kuwa Kamati ya Utendaji ndiyo iliyomkaimisha nafasi hiyo na ndiyo iliyoamua kutengua, hivyo wanazo sababu zao za msingi.
Pia Shaka alisema kuwa nafasi hiyo itajazwa baada ya kukamilika kwa taratibu za kikanuni na mamlaka husika kufanya uamuzi kupitia vikao vyake.
Jokate amekaimu nafasi hiyo tangu Aprili mwaka jana alipoteuliwa na Uteuzi wake ulizua malalamiko kutoka kwa baadhi ya wanachama waliodai taratibu hazikufuatwa ipasavyo.