Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka wafanyabiashara wilayani Ruangwa kutumia taasisi za kifedha kukopa fedha kwa ajili ya kukuza mitaji yao.

Ameyasema hayo jana wakati akizungumza na wafanyabiashara wa wilaya hiyo katika kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Chama Cha Walimu, wilayani Ruangwa.

Waziri Mkuu ambaye yuko wilayani Ruangwa kwa ziara ya kikazi ya siku mbili amesema ni vema wakatumia taasisi za kifedha zilizopo ili kukuza mitaji yao.

Amesema katika kuhakikisha riba zinapungua, Rais Dkt. John Magufuli anaendelea kuzungumza na wamiliki wa taasisi za kifedha ili waone namna ya kupunguza riba hiyo.

Waziri Mkuu amesema lengo la Serikali la kuchukua hatua hiyo ni katika kutekeleza mkakati wake wa  kuwawezesha wafanyabiashara ili waweze kupata mikopo yenye riba nafuu.

Pia Waziri Mkuu amewahakikishia wananchi wa wilaya hiyo kwamba Serikali ipo pamoja nao na imedhamilia kuboresha huduma mbalimbali za jamii kama maji na afya.

Naye, Mwenyekiti wa Umoja wa Wafanyabiashara wa Wilaya ya Ruangwa, Bw. Said Shea amewaomba wafanyabiashara wenzake watumie fursa za maendeleo zilizoko wilayani humo kwa kupanua wigo wa biashara zao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *