Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalif Seif Sharif Hamad amemtolea uvivu Mwenyekiti wa Chama hicho anayeungwa mkono na Msajili wa Vyama vya siasa, Prof. Ibrahimu Lipumba akimtaka kuacha kukivuruga chama hicho kwani muda walionao kwa sasa ni kukijenga chama hicho.
Maalim ameyasema hayo wakati wa mkutano wake na wanachama wa chama hicho uliofanyika katika Hoteli ya Korini iliyopo Tandale jijini Dar es Salaam ambapo amewataka wanachama wake kuwa wamoja na kutoyumbishwa na upande wa Lipumba.
Amesema kuwa Lipumba ni mtu asiyekuwa mkweli, kwani yeye ndiye aliyempokea Edward Lowassa katika UKAWA lakini siku chache baadae aligeuka na kudai kuwa hakubaliani na maamuzi ya kumkaribisha katika umoja huo.
Mkutano baina ya Katibu mkuu wa chama hicho na wanachama hao ulikuwa na lengo la kujenga mshikamano na umoja ndani ya chama hicho.