Upelelezi wa kesi ya utakatishaji fedha inayomkabili Rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva na makamu wake Godfrey Nyange umekamilika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Wakili wa serikali, Nassoro Katuga amemueleza Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa kesi hiyo imeitishwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake umekamilika.
Wakili Katuga ameiomba mahakama iahirishe kesi hiyo hadi tarehe nyingine ili kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali (PH).
Pia ameeleza kuwa mshtakiwa wa kwanza Avave bado anaumwa na amelezwa Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi April 5,2018 kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali (Ph).
Mbali ya Aveva katika kesi hiyo mshtakiwa mwingine ni Godfrey Nyange ‘Kaburu’ ambaye ni Makamu wa Rais wa Klabu ya Simba.
Kwa pamoja washtakiwa wanakabiliwa na Mashtaka matano ya uhujumu uchumi ikiwamo kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo na utakatishaji fedha ambazo ni Dola za Marekani (USD) 300,000.