Mkuu wa Magereza nchini, Kamishna Jenerali Dk. Juma Malewa, amesema Jeshi hilo limeanza kufanyia kazi agizo la Rais John Magufuli la kuhakikisha wanajitosheleza kwa chakula na kulisha wafungwa.

Amesema hatua hiyo itaondoa utaratibu wa wafungwa kupelekewa chakula kutoka nje, kwa kuwa watakuwa wanakula wanachokizalisha wakiwa magerezani.

Dk. Malewa alisema hayo katika mkutano wa maafisa waandamizi wa Jeshi la Magereza kutoka maeneo mbalimbali kuweka mkakati wa namna ya kufanikisha agizo hilo la Rais alilolitoa akiwa mkoani Dodoma hivi karibuni.

Rais Magufuli alilitaka jeshi hilo kuhakikisha linawatumia wafungwa kuzalisha chakula kwa ajili ya kuwalisha badala ya kutegemea ruzuku ya serikali kwa chakula.

Alisema kwa sasa Jeshi hilo lina uwezo wa kujitosheleza kwa chakula kwa asilimia 30, kutokana na vifaa vichache vilivyopo, lakini wanatarajia kupokea na kuongeza vifaa zaidi yakiwamo matrekta ili kuongeza nguvu zaidi ya uzalishaji na kufikia asilimia 100 ya kujitosheleza kwa chakula.

Malewa alibainisha mkakati wa kuhakikisha Magereza inatumika kama chuo cha mafunzo kwa kuwafundisha wafungwa mbinu mbalimbali za kilimo ili wote watumike vyema na kwa ufanisi katika kuboresha sekta ya kilimo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *