Ufilipino imesema itajiondoa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), mwezi mmoja tangu mwendesha mashtaka mkuu alipotangaza kuanzisha uchunguzi wa vita tata dhidi ya dawa za kulevya iliyosimamiwa na Rais Rodrigo Duterte.
Msemaji wa Duterte Harry Roque amesema katika taarifa ya Jumatano kwamba nchi imetoa taarifa itajitoa kwenye mkataba wa Rome, Italia ulioanzisha mahakama hiyo yenye makao yake The Hague, Uholanzi.
Duterte amekuwa akishtumiwa kwa kuhimiza mauaji ya kiholela na ukiukwaji mwingine wa haki katika jitihada zake za kuondokana na dawa za kulevya katika nchi hiyo tangu alipoingia madarakani baada ya uchaguzi wa mwaka 2016.
Februari mwaka huu, ICC ilitangaza kuwa itaanzisha uchunguzi wa awali ili kuamua kama uchunguzi wa kina utahitajika.
Roque amesema Duterte atakaribisha uchunguzi kwa sababu “anasikitishwa na amechoka kushtumiwa … (na) tume ya uhalifu dhidi ya ubinadamu.”