Kiongozi wa ODM, Raila Odinga amewaomba wabunge kutoka chama chake kuunga mkono majadiliano yaliyofikiwa katika kikao cha Ijumaa kati yake na Rais Uhuru Kenyatta.
Odinga aliwataka wabunge hao wasiyumbishwe na watu waliojipanga kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.
Aliwaambia wabunge wa chama hicho kwamba mkutano uliofanyika kwenye Ofisi za Rais zilizoko Jengo la Harambee Ijumaa iliyopita ni matokeo ya tukio la Januari 30 ambapo Raila aliapa kama rais wa watu.
Aliwahimiza kutumia kikamilifu fursa ya mpango uliofikiwa ili kuhakikisha mazungumzo ya kitaifa yanaanza.
Aliwaambia wabunge kuwa mabadiliko ya mwelekeo yalikuwa muhimu ikiwa chama hicho kinataka kunufaika na ushindani wa siasa siku zijazo.
Raila alizungumzia hata mvutano uliosababisha mgawanyiko wa upinzani ndani ya Bunge wakati wanachama wengine wa Nasa walipigania nafasi za uongozi zilizotengwa kwa ajili ya wapinzani.
Ili kuonyesha dhamiri yake kwa mkutano kati ya Rais Kenyatta na Raila, chama hicho kiliandamana hoja ya kutafuta msaada wa mabunge yotw mawili ili kupitisha ajenda yenye hatua tisa ambazo viongozi wawili hao walikubaliana baada ya mkutano wao wa Ijumaa iliyopita.