Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan jana amekutana na kuzungumza na Balozi mpya wa Ufaransa nchini Frederic Clavier.

Katika mazungumzo hayo ambayo yalifanyika Ofisini kwa Makamu wa Rais, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Balozi huyo mpya wa Ufaransa nchini ambaye amekutana na kuzungumza na Mheshimiwa Makamu wa Rais aliipongeza Tanzania kwa kuwa mstari wa mbele katika masuala mbali mbali ya Kimataifa.

Balozi alimjulisha Makamu wa Rais kwamba Ufaransa imekusudia kuimarisha uhusiano zaidi na Tanzania wa Uchumi na Siasa na kuanzisha majadiliano mbali mbali katika masuala ya Mazingira,Mabadiliko ya Tabia Nchi.

Balozi Clavier alimjulisha Makamu wa Rais kuwa mwezi ujao kutakuwa na ugeni wa wafanya biashara kati ya 30 au 40 kutoka nchi ya Ufaransa ambao watakuja kujionea fursa mbali mbali za kibiashara na uwekezaji zinazopatikana nchini Tanzania.

Balozi alimuelezea Makamu wa Rais azma ya Ufaransa kushirikiana na Vyuo Vikuu vya Tanzania katika kuanzisha na kuendesha kozi mbali mbali kwa manufaa ya pande zote mbili.

Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan alimshukuru na kumpongeza Balozi wa Ufaransa kwa kazi nzuri wanazofanya hapa nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *