Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amewataka wakandarasi wazawa wanaopata kazi katika miradi mbalimbali inayotolewa na serikali, kuhakikisha kuwa wanatumia bidhaa za ndani kabla ya kutumia bidhaa za nje.

Rais Magufuli ameyasema hayo jana, wakati akifungua kiwanda cha kutengeneza mabomba ya plastiki, mabati pamoja chuma kinachomilikiwa na Kahama Oil Mill kilichopo Mjini Kahama.

Amesema, kila mkandarasi hapa nchini anatakiwa kutumia bidhaa zinazotengenezwa hapa nchini katika shughuli zake na kuongeza kuwa bidhaa zinapoisha na shughuli zake bado zinaendelea anatakiwa kupata kibali cha kuagiza bidhaa kutoka nje.

Hata hivyo alizitaka taasisi za fedha zikiwemo benki kuhakikisha zinapunguza riba kwa wafanyabiashara na kuongeza kuwa awali mabenki mengine yalikuwa yanatoza riba kubwa mpaka asilimia 25 hali ambayo wawekezaji wa viwanda wanashidwa kujiendesha na kujikuta yanapata hasara huku akisema kwa sasa jumla ya viwanda 3600 tayari vimekwisha funguliwa nchini.

Wakati huo huo, Rais Magufuli aliwataka wawekezaji kutumia malighafi zinazopatikana hapa nchini hususani madini ya chuma hali itakayowafanya kuzalisha bidhaa zao kwa faida kubwa kuliko kuendelea kutumia malighafi kutoka nje. Mkurugenzi wa Kiwanda cha Kahama Oil Mill, Mhoja Nkwambi alisema kuwa kiwanda hicho kilianzishwa mwaka 2002 nakutoa ajira 720 huku 120 zikiwa ajira za kudumu na 600 zikiwa ajira za muda mfupi kulingana na upatikanaji wa malighafi.

Alisema, amekuwa akipata changamoto za uuzaji wa bidhaa anazozalisha kutokana na bidhaa zinazotengenezwa nje kuingia kwa wingi nakupelekea bidhaa zinazotengezwa ndani kukosa soko hata kama zinakidhi ubora. Nkwambi alisema serikali ithamini bidhaa zinazotengenezwa ndani badala ya kutoa kipaumbele kwa bidha zinazotoka nje ya nchi na kuvilinda viwanda vya ndani ili viweze kujiendesha na kupata mikopo ya riba fuu kutoka katika mabenki na tasisisi mbalimbali za kifedha.

Pia Mkurugenzi huyo aliiomba serikali kumsaidia kupata soko la mabomba ya plastiki, mabati na vyuma hapa nchini ili wanunuzi waache kuagiza bidhaa hizo kutoka nje na kwamba, hali hiyo itasida kuvilinda viwanda katika ushindani wa kibishara katika masoko ya ndani na nje.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *