Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir amewaomba wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kusaidia kupatikana kwa amani ya kudumu nchini kwake.

Kiongozi huyo wa Sudan Kusini ametoa ombi hilo wakati wa mkutano wa 19 wa Wakuu wa Nchi za EAC jijini Kampala, Uganda.

Ametumia nafasi hiyo kuwaomba rasmi viongozi wa EAC kuongeza juhudi zao za amani ya kudumu katika nchi za Sudan Kusini, Burundi na DRC, akisisitiza vita na migogoro ya mara kwa mara inachangia kurudisha nyuma maendeleo ya ukanda wa jumuiya hiyo yenye nchi sita ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini.

Aligusia pia umuhimu wa EAC kuiunga mkono Sudan Kusini ili ichangie maendeleo katika sekta za miundombinu, afya na nyinginezo ndani ya jumuiya.

Mwenyekiti wa EAC, Rais Yoweri Museveni wa Uganda aliwataka wakuu wengine wa nchi za jumuiya hiyo kuwaunganisha raia wake zaidi ya milioni 160 na miradi ya uwekezaji wa ndani katika miundombinu ili kukuza tija katika uzalishaji na mengineyo.

Wakati huohuo, Waziri anayeshughulikia nishati ya Petroli Sudan Kusini, Ezekiel Gatkouth amepinga pendekezo la kumtaka Rais Kiir aachie ngazi ili kupisha mchakato wa amani nchini hapa ikiwa ni pamoja na kuandaa uchaguzi mkuu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *