Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amezindua kiwanda cha Inhemeter ambacho kitakuwa kinazalisha mita za luku na kuziuza kwa mashirika ya ugavi wa umeme nchini.
Kiwanda hicho ambacho ni cha kwanza kujengwa hapa nchini na cha nne Afrika kina soko la uhakika la kuuza mita 500,000 kwa mwaka kwa Shirika la Umeme nchini (Tanesco), Wakala wa Umeme Vijijini (Rea) na Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco).
Mwijage aliyataka mashirika hayo kutumia fursa ya kuwepo kwa kiwanda hicho kuboresha huduma zao huku akisisitiza kwamba kitakuwa na manufaa mengi ikiwemo ajira kwa vijana 100 na mashirika kutotumia fedha za kigeni kuagiza mita nje ya nchi.
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kujenga uchumi wa kati na viwanda ifikapo 2025 na kuzinduliwa kwa kiwanda cha Inhemeter ni uthibitisho kuwa azma hiyo imeshaanza kutekelezwa kwa vitendo.
Pia alisema anayo furaha kushuhudia uzinduzi wa kiwanda kipya cha 3,307 katika kipindi kifupi.
Awali, akizungumza kwenye hafla hiyo, Mshauri Mkuu wa kiwanda hicho ambaye pia ni katibu mkuu mstaafu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dk Adelhem Meru alivishauri vitengo vya manunuzi nchini kusaidia ujenzi wa viwanda.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho, Abraham Rajakili alisema Inhemeter ni kampuni yenye uzoefu wa miaka 20 katika tafiti, uzalishaji na usambazaji wa mita za luku na tayari wameshasambaza katika zaidi ya nchini 60 dunia.