Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Lipumba amesema chama hicho hakina nguvu visiwani Zanzibar kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma kwa sababu ya uamuzi mbaya kiliouchukua wa kususia uchaguzi wa marudio.

Akizungumza katika mkutano wa ndani wa chama hicho uliofanyika katika ukumbi wa Makonyo Chake Chake Pemba, Profesa Lipumba alisema nguvu ya CUF haipo tena kwa sababu hakipo katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).

Alimtuhumu Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kuwa chanzo kwa uamuzi wake wa kubariki kutoshiriki uchaguzi huo, jambo lililokifanya kikose sifa za kuwamo katika serikali hiyo.

Wakati Profesa Lipumba akieleza hayo, Nassor Ahmed Mazrui ambaye ni naibu katibu mkuu wa CUF Zanzibar upande unaomuunga mkono Maalim Seif, alisema hawatambui ziara hiyo kwa maelezo kuwa mwenyekiti huyo si kiongozi wao.

Januari 28, 2016 Baraza Kuu la Uongozi la CUF lilitangaza kutoshiriki uchaguzi wa marudio visiwani Zanzibar uliotangazwa na Tume ya Uchaguzi (ZEC), likitoa hoja 12 za uamuzi huo.

 

Uchaguzi huo wa marudio wa rais wa Zanzibar, wawakilishi na madiwani ulifanyika Machi 20, 2016.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *