Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ametoa wito kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kusimamia vizuri rasilimali walizonazo.
Rais Magufuli ametoa wito huo jana mjini Kampala nchini Uganda wakati akichangia katika mkutano wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unaojadili maendeleo na upatikanaji wa fedha kwa ajili ya miradi ya sekta ya miundombinu na afya.
Taarifa hiyo imechangiwa na wadau mbalimbali wakiwemo Marais, wawakilishi wa sekta binafsi na washirika wa maendeleo ambao wameelezea njia mbalimbali za kupata fedha za kutekeleza miradi hiyo ikiwemo kutumia mfumo wa ushirikiano kati ya Serikali na Sekta binafsi (PPP).
Katika mchango wake Rais Magufuli amesema pamoja na kutumia mfumo wa PPP ni muhimu kwa Serikali za kila nchi kusimamia vizuri ukusanyaji wa mapato ya kodi na rasilimali nyingine ili kutekeleza miradi ya miundombinu, afya na sekta nyingine.
Ametahadharisha kuwa japo kuwa mfumo wa PPP ni mzuri, ni vyema wataalamu wakachukua tahadhali za kutosha ili kuepusha Serikali kuingia katika mikataba isiyokuwa na maslahi kwa nchi zao kutokana na baadhi ya wadau wa sekta binafsi kutaka kutengeneza faida kubwa kwa kupandisha gharama za miradi.
Rais Magufuli ametolea mfano wa miradi mikubwa iliyoanza kutekelezwa nchini Tanzania ukiwemo ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) na ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stieglers’ Gorge), kuwa Serikali ya Tanzania imeamua kuanza kutekeleza miradi hiyo kwa kutumia fedha zake baada ya kufanikiwa kusimamia vizuri rasilimali zake na kubana matumizi.
Marais waliohudhuria mkutano huo ni Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Kenya, Uhuru Muigai Kenyatta, Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir Mayardit na Marais wa Rwanda na Burundi wamewakilishwa.