Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka Watanzania wakiwemo wakazi wa mkoa wa Mwanza kuachana na biashara ya dawa za kulevya.
Pia Waziri Mkuu amegiza vijana nchini waelimishwe madhara mbalimbali yanayosababishwa na matumizi ya dawa za kulevya ili wajiepushe nazo.
Waziri Mkuu aliyasema hayo jana (Jumanne, Februari 20, 2018) alipozindua kliniki ya methadone kwa ajili ya waathirika wa dawa za kulevya.
Alizindua kliniki hiyo iliyopo kwenye hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mwanza ya Sekou Toure akiwa katika siku ya sita ya ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza.
Pia aliwaomba wananchi washirikiane na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na dawa hizo.
Kwa upande wake, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Bw. Rogers Siyanga aliishukuru Serikali kwa kutambua madhara ya dawa za kulevya na kuchukua hatua.