Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imesema imebaini kuwa kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF) linaloongozwa na Askofu Zacharia Kakobe linatunza kiasi kikubwa cha fedha kwenye ndoo kinyume na taratibu za utunzaji fedha.

Imeelezwa pia utoaji wa kiwango kikubwa cha pesa katika akaunti za benki haushirikishi vyombo vya ulinzi na usalama kwaajili ya usalama wa fedha na wahusika.

Vile vile kanisa hilo halitengenezi hesabu za mapato na matumizi ya fedha jambo linalosababisha matumizi mabaya ya fedha hizo.

Akitoa taarifa hiyo Kamishna Mkuu wa TRA Charles Edward Kichere ameeleza kuwa Askofu Kakobe hana akaunti ya fedha katika taasisi yoyote hapa nchini na ni mmoja wa wasimamizi wakuu wa akaunti ya kanisa lake ambazo zina jumla ya kiasi cha Tsh Bilioni 8.13.

Kiasi hicho kimetokana na sadaka, zaka na changizo zinazotolewa na waumini hivyo kwa mujibu wa sheria havitozwi kodi na kutokana na uchunguzi uliofanya kanisa hilo limekwepa kulipa kodi ya Tsh Milioni 20.8 katika shughuli zake za kiuchumi lakini imelipwa baada ya uchunguzi.

Kamishna Kichere ameeleza pia kuwa fedha za kanisa zinatumika kujenga nyumba ya mke wa Askofu Kakobe kwa jina lake na sio kwa jina la kanisa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *