Idara ya uhamiaji nchini imewataka watanzania kupuuza habari zinazozagaa kuhusu uvumi wa pasipoti mpya kuwa zimechakachuliwa.
Kauli hiyo imetolewa jana na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji nchini, Dkt. Anna Makakala jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema wananchi wanatakiwa kupata taarifa sahihi kila mara juu ya kila jambo linalohusu maendeleo yao na mambo yanayoletea ustawi wa Taifa , na kwamba wao Idara ya Uhamiaji ndio wenye taarifa sahihi zinazohusu Mchakato mzima wa Pasipoti Mpya za Kielektroniki
Hivi karibuni Rais Dkt. John Magufuli wakati akizindua hati mpya za kusafiria alisema kumekuwapo na wahujumu wa mchakato huo ambao hawakufanikiwa kuiba sh. bilioni 400.
Alisema kumekuwapo na watu waliozunguka kila kona na kutumia kila njama zote kupiga vita mchakato huo wakidhani watafanikiwa kuhujumu serikali.
Dkt. Anna Makakala alisema hatua hizo za kutoa na kueneza taarifa zisizo sahihi zinawaletea mkanganyiko wananchi na kudhoofisha mawazo na fikra chanya kwa Taifa lao
Alisema ni vyema jamii ikatambua kuwa mchakato wa Pasipoti mpya ya kidigitali ni hatua kubwa kwa Taifa hili na si vyema kuutolea Taarifa zisizo sahihi. Aliwasihi wanahabari kupata taarifa kutoka katika vyanzo sahihi na kuzifikisha kwa walaji ambao ni Wananchi.
Alisisitiza hatua ya mafanikio ya matumizi ya hati hizo hazitarudi nyuma kwa sababu ya kuwapo na taarifa zisizo sahihi zenye lengo la kupotosha ukweli wa mchakato huo.