Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imetangaza bei mpya za mafuta zinazoanza kutumika leo huku bei za petroli, dizeli na mafuta ya taa zikipanda.
Taarifa kwa umma iliyotolewa leo na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Nzinyangwa Mchany imesema bei za rejareja zimeongezeka kwa petroli ikiwa ni Sh59 sawa na asilimia 2.70, dizeli Sh46 (sawa na asilimia 2.30), na mafuta ya taa kwa Sh24 (sawa na asilimia 1.17).
Amesema bei za jumla nazo zimeongezeka ambazo kwa petroli ni Sh58.57 sawa na asilimia 2.85, dizeli kwa Sh46.48 (sawa na asilimia 2.44) na mafuta ya taa kwa Sh23.75 (sawa na asilimia 1.24).
Amesema bei za rejareja katika mikoa ya Kaskazini zimeongezeka, ambazo petroli ni kwa Sh15 sawa na asilimia 0.70 na dizeli kwa Sh47 sawa na asilimia 2.29. Bei za jumla zimeongezeka petroli ikiwa ni kwa Sh15.36 sawa na asilimia 0.73 na dizeli Sh47.18 sawa na asilimia2.42.
Kaimu mkurugenzi mkuu huyo amesema sehemu ya shehena kubwa ya mafuta yaliyopokewa katika Bandari ya Dar es Salaam ni yenye bei ya soko la dunia za Novemba, 2017 wakati iliyopokewa katika Bandari ya Tanga ni ya bei ya soko la dunia ya Desemba 2017.
Amesema bei za mafuta katika soko la dunia kwa Novemba 2017 ziko juu kwa zaidi ya asilimia sita ikilinganishwa na bei za Oktoba 2017, wakati bei za Desemba zina mabadiliko tofauti.
Amesema bei ya petroli imepungua kwa asilimia 0.2 na ya dizeli na mafuta ya taa imeongezeka kwa asilimia 2.7 na asilimia 1.9.