Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimemtaka mgombea udiwani katika kata ya Buhangaza wilayani Muleba kujiondo kwenye kinyang’anyiro hicho cha uchaguzi.
Maamuzi hayo yanakuja kufuatia kutekwa kwa mgombea huyo na watu wasiojulikana kwa zaidi ya siku mbili.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dtk. Vincent Mashinji huku akisema jeshi la polisi linatakiwa kufanya uchunguzi wa haraka ili kubaini waliomteka mgombea huyo wa udiwani.
Mashinji amesema kuwa Makoti alitekwa Februari 2 mwaka huu katika mazingira ya kutatanisha na kupatikana Februari 5 akiwa ametelekezwa eneo la Hospitali ya Kagando iliyoko Muleba ambako mpaka sasa ndipo amelazwa.
Pia amesema kuwa watekaji walimteremsha katika bodaboda aliyokuwa amepanda wakati akitokea kwenye mchakato wa kampeni za udiwani ambapo watekaji hao walikuwa ndani ya gari aina ya Toyota RAV 4.
Ameongeza kuwa Makoti alitakiwa kukukubali kupokea pesa ambazo walikuwa nazo ili aweze kujitoa katika kinyang’anyiro hicho cha udiwani lakini baada ya kukataa ndipo alianza kusulubiwa hadi hapo walipotimiza azima yao.