Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli  amezindua Kituo cha Mafunzo Maalum ya Kijeshi (Comprehensive Training Center – CTC) kilichopo Mapinga katika Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani.

Kituo hicho kimejengwa kwa msaada kutoka Jeshi la Ukombozi la Watu wa China kwa gharama ya Shilingi Bilioni 67.87 na kitatumika kutoa mafunzo ya kijeshi ya kisasa yatakayowawezesha askari kukabiliana na vitisho vya kisasa vya kiusalama.

Kabla ya kuzindua kituo hicho Mhe. Rais Magufuli na Balozi wa China hapa nchini Mhe.  Wang Ke wameshuhudia makabidhiano ya kituo hicho kutoka Jeshi la Ukombozi la Wananchi wa China lililowakilishwa na Naibu Mkuu wa Idara ya Mafunzo na Utawala ya Kamisheni Kuu ya Jeshi hilo Jenerali Yang Jian kwenda kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lililowakilishwa na Meja Jenerali Yakub Hassan Mohamed.

Mhe. Rais Magufuli pia ameshuhudia mazoezi ya kijeshi yaliyofanywa katika kituo hicho yakiwemo shambulizi la kutokea baharini (amphibian landing), makomandoo kukabiliana na magaidi na kupiga shabaha kwa kutumia miundombinu ya kisasa.

Akizungumza na Maafisa, Askari na wananchi waliojitokeza kushuhudia tukio la makabidhiano ya kituo hicho Mhe. Rais Magufuli amelishukuru Jeshi la Ukombozi la Watu wa China na Serikali ya China kwa kutoa msaada wa kujengwa kwa kituo hicho na amesema Serikali ya Awamu ya Tano inathamini na kutambua mchango wa China katika Jeshi la Ulinzi la wananchi wa Tanzania.

Mhe. Rais Magufuli amesema China imeendelea kudhihirisha urafiki na udugu wake na Tanzania kwani licha ya kujenga kituo hicho pia imetoa msaada wa kujenga kituo cha mafunzo ya kijeshi ya anga cha Ngerengere Mkoani Morogoro na miradi mingine ya maendeleo ya jamii na hivyo amemuomba Balozi wa China hapa nchini Mhe. Wang Ke kufikisha shukrani zake kwa Rais wa China Mhe. Xi Jinping.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *