Rais wa Afrika kusini anakabiliwa na shinikizo zaidi kujiuzulu kufuatia mazungumzo na maafisa wa ngazi ya juu katika chama chake cha ANC.

Haijafichuliwa mazungumzo hayo yalihusu nini lakini viongozi katika chama hicho wanatarajiwa kufanya mkutano wa dharura hii leo Jumatatu.

Cyril Ramaphosa aliichukuwa nafasi ya kiongozi wa chama cha ANC kutoka kwa Zuma, anayekabiliwa na tuhuma za rushwa.

Wachambuzi wanasema wakuu wa chama hicho wanajaribu kuondoa mvutano wa kung’ang’ania madaraka ambao unaweza kukigawanya chama hicho kabla ya uchaguzi mkuu mwakani.

Wanatarajiwa kuanza mchakato wa kumuondoa rais Zuma kupitia mfumo rasmi wa kumuondoa au kwa kuidhinisha hoja bungeni.

Maafisa sita wakuu wa chama hicho tawala waliwasili mmoja baada ya mwingine Jumapili katika makaaziya Zuma mjini Pretoria.

Walinyamaza kimya wakati mazungumzo yalipomalizika lakini wameitisha mkutano wa kamati kuu ya chama hicho Jumatatu.

Julius Malema, kiongozi wa upinzani na aliyekuwa mafuasi wa chama hicho cha ANC alisema kwenye mtandao wake wa Twitter kwamba rais Zuma amekataa kujiuzulu.

Zuma anastahili kusalia madarakani hadi uchaguzi mwaka ujao 2019. Hatahivyo chama hicho kimepoteza umaarufu wake katika muhula wa pili wa kiongozi huyo huku kukishuhudiwa pia kudorora kwa uchumi na tuhuma za rushwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *