Mtoto mkubwa wa kiume wa aliyekuwa kiongozi wa mapinduzi na baadaye Rais wa Cuba Fidel Castro, Fidel Castro Diaz-Balart amejiua baada ya kupatiwa matibabu kwa muda mrefu wa msongo wa mawazo.
Fidel au Fidelito ambaye ni mtoto wa kwanza wa aliyekuwa kiongozi huyo maarufu duniani kutokea Cuba, alikuwa na umri wa miaka 68, alikutwa akiwa amefariki siku ya Alhamisi, alikuwa mtaalamu wa masuala ya Nyuklia, na anatajwa kufanana sana na baba yake marehemu Fidel Castro.
Fidelito ambaye anaheshimiwa sana na watu wa Cuba alizaliwa 1949, na Mirta Diaz-Balart ambaye alikuwa ni binamu wa maadui wakubwa wa Fidel Castro, Mario Diaz-Balart congressman Lincoln Diaz-Balart, hivyo alikuwa kama mtu pekee anayefanya familia hizo kuwa ndugu.
Fidelito alikuwa akifanya kazi kama mshauri wa masuala ya kisayansi wa Rais wa sasa wa Cuba, Raul Castro ambaye ni baba yake mdogo, aliyechukua madaraka baada ya baba yake mzazi kuwa mgonjwa, na pia ni Makamu wa Rais wa Chuo cha Sayansi cha Cuba.