Baada ya mahakama ya wilaya ya Ilala kumuhukumu kwenda jela miaka saba mtuhumiwa Salum Njwete ‘Scorpion’ hatimaye mlalamikaji Said Mrisho hajakubaliana na hukumu hiyo.
Leo Mahakama ya Wilaya ya Ilala imemuhukumu Scorpion miaka 7 jela baada ya kupatikana na hatia ya kumjeruhi na kumsababishia upofu Said Mrisho.
Mnamo Septemba 6, 2016 saa 4 usiku maeneo ya Buguruni Dar es salaam, Scorpion alifanya tukio la unyang’anyi ambapo aliiba cheni ya Silva yenye uzito wa gramu 34 ikiwa na thamani ya Sh 60,000, simu ya mkononi na fedha taslimu Shilingi 330,000 vyote vikiwa na thamani ya Sh 474,000 mali ya Said Mrisho.
Inadaiwa kuwa kabla na baada ya kufanya tukio hilo, Scorpion alimchoma visu Mrisho sehemu mbalimbali za mwili ikiwemo machoni, tumboni na mabegani ili kurahisisha kupata mali hizo.
kufuatia tukio hilo Said Mrisho ambaye mpaka sasa hana uwezo wa kuona baada ya kutobolewa macho yake yote mawili ameamriwa na mahakama kulipwa faini ya milioni 30 kama namna ya fidia.
Hakimu Haule amesema katika hukumu hiyo Mahakama ilijikita sehemu kuu tatu ikiwemo kama mlalamikaji, Said Mrisho amepata majeraha ya hatari pamoja na kama Scorpion alitumia unyang’anyi wa kutumia silaha.
Hata hivyo Said Mrisho ameonekana kutoridhishwa na hukumu hiyo ya miaka ya 7 na kusema ni ndogo hivyo atapeleka ombi lake kwa Rais Magufuli.