Umoja wa Afrika umemtaka Rais wa Marekani, Donald Trump kufika katika kikao cha umoja huo kitakachofanyika nchini Ethiopia mwezi huu kutokana na matamshi ya kibaguzi anayodaiwa kuyatoa hivi karibuni kuhusu nchi za Afrika.

Trump anadaiwa kuziita nchi za Afrika kuwa ni ‘shimo la choo’ (shithole) alipokuwa kwenye mkutano wa ndani uliolenga kujadili sera ya uhamiaji inayowapa nafasi zaidi wahamiaji vijana kutoka Afrika na Haiti kuingia nchini Marekani.

Kwa mujibu wa BBC, Baadhi ya mabalozi wa nchi za Afrika wamekutana na Balozi wa Marekani kwa Umoja wa Mataifa, Nikki Haley ambaye ameeleza kusikitishwa na kinachoendelea kujadiliwa kuhusu mkutano uliofanyika Ikulu ya Marekani.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, Balozi wa Afrika Kusini kwa Umoja wa Mataifa, Jerry Matjila aliyezungumza kwa niaba ya mabalozi wengine alimueleza Haley kuwa itakuwa na maana zaidi kama Trump atafika mbele ya kikao cha Umoja wa Afrika kinachofanyika Addis Ababa kuanzia Januari 28, kutoa ufafanuzi.

Hata hivyo, Haley amewaeleza kuwa hafahamu kwa uhalisia ni nini hasa kilichozungumzwa na Trump kwenye kikao hicho kilichofanyika Ikulu ya Marekani wiki iliyopita, lakini ataufikisha ujumbe wao kwa Trump kwani atakutana naye hivi karibuni jijini Washington.

Kupitia akaunti ya Twitter ya Ujumbe wa Marekani kwa Umoja wa Mataifa, imewashukuru wajumbe wa umoja huo kutoka Afrika kwa kufanya nao mkutano.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *