Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametoa agizo kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Januari Makamba kuunda Kamati ya pamoja ya wataalam kutoka Tanzania Bara na Zanzibar ili kupitia upya usajili wa meli nchini.

Makamu wa Rais ametoa agizo hilo mbele ya Waandishi wa Habari jana Jijini Dar es Salaam, alipokuwa akitoa ufafanuzi juu ya meli zilizokamatwa zikiwa na Bendera ya Tanzania.

Mhe. Samia amesema kuwa suala la usajili wa meli za nje ni la kawaida na linafanywa na nchi nyingi duniani hivyo Serikali inaendelea kushughulikia taarifa juu ya meli za nje zilizosajiliwa Tanzania zenye tuhuma za kusafirisha silaha na dawa za kulevya kwa sababu ni kinyume cha sheria.

Kamati itakaundwa pia itapitia sheria za usajili wa meli ili kuzipa nguvu zaidi taasisi zinazosimamia usajili huo hivyo kamati itaangalia kwa makini kodi zinazotozwa na mchango wake nchini ili zisiwe kivutio kwa meli zisizokidhi viwango kuomba usajili Tanzania.

Samia amsema agizo lakupitiwa upya sharia za usajili wa meli baada ya kubainika kuwa wamiliki wa meli wanapenda kusajili meli zao nje ya nchi zao kukimbia ukubwa wa kodi na sheria zinazobana pia wakala aliyekuwa akifanya kazi hizo kwa niaba ya taasisi ya Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) alishavunjiwa mkataba lakini bado anaendelea kufanya usajili kwa kuiba bendera ya Tanzania.

Amefafanua kuwa Sheria na Kanuni zote za usajili zinamlazimu mimiliki wa meli kujaza fomu ya kiapo cha kutovusha biashara za dawa za kulevya wala silaha kinyume na utaratibu hivyo Watanzania wanatakiwa kuelewa kuwa kukamatwa kwa meli hizo sio makosa ya Tanzania ila nchi inahusishwa kwa kuwa usajili wa meli hizo umefanyika Tanzania.

Meli mbili, Kaluba yenye namba za usajili IMO 6828753 na Andromeda yenye namba za usajili IMO 7614666 zilizosajiliwa Tanzania kupitia taasisi ya Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) zilikamatwa kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya na silaha ambapo hadi sasa tayari zimeshachukuliwa hatua ya kufutiwa usajili.

Tanzania ina aina mbili za usajili wa meli ambao ni usajili wa meli zenye asili ya Tanzania na zisizo asili ya Tanzania, usajili huo ni kwa mujibu wa mkataba wa UNCLOS wa mwaka 1982 ambapo kila nchi imepewa haki ya kufanya usajili wa meli kwa kuzingatia mikataba ya kimataifa na sheria za nchi husika.

SUMATRA inaruhusu usajili wa meli zinazomilikiwa na Watanzania au kwa ubia kati ya Mtanzania na raia wa nchi nyingine ambapo jumla ya meli 88 zimesajiliwa wakati meli za kimataifa zinasajiliwa Tanzania kupitia Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) ambazo hadi Disemba 31, 2017 jumla ya meli 457 za nje zimesajiliwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *