Kesi ya kutumia dawa za kulevya inayomkabili Agnes Gerald maarufu kama ‘Masogange’ inaonekana kuwa na vizingiti baada ya upande wa utetezi kushindwa kutoa ushahidi wake.
Kufuatia tukio hilo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewaonya upande wa utetezi kwa kushindwa kutoa ushahidi wao kwa mara ya tatu mfululizo, baada ya wakili wa utetezi, Nehemia Nkoko kudai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri kuwa wakili mwenzake, Reuben Simwanza ndiye aliyeandaa mashahidi lakini ameshindwa kutokea kwa kuwa anaumwa, hivyo atahakikisha anaandaa mashahidi, na itakapotokea wakili mmoja hayupo mwengine aendelee na shauri.
“Hatuna pingamizi na sababu zilizotolewa na upande wa utetezi lakini tunaomba Mahakama itambue kuwa ni mara ya tatu kwa upande wa utetezi inaahirishwa kesi hii? Mawakili wapo wengi lakini wanashindwa kuendelea kutoa ushahidi wao wa upande wa utetezi basi kama hawawezi, waache mshitakiwa aendelee na kesi mwenyewe.” amesema wakili Kakula wa upande wa mashtaka
Kutokana na hali hiyo, upande wa mashtaka umeomba ahirisho la mwisho kwa sababu kesi ni ya muda mrefu, na kesi hiyo kuahirishwa hadi Januari 26, mwaka huu kwa ajili ya kusikilizwa, ambapo Masogange ataanza kujitetea baada ya Mahakama kumkuta na kesi ya kujibu.