Mchezaji wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo amesema kuwa hana furaha Real Madrid na anataka kurejea kwenye klabu yake ya zamani Manchester United.
Ronaldo amekasirishwa na kitendo cha uongozi wa klabu hiyo kushindwa kuzungumza naye ili kuongeza mkataba wake.
Kwa mujibu wa magazeti ya Hispania ni kuwa Rais wa klabu hiyo, Florentino Perez alimwahidi kumwongeza mshahara mapema lakini ameshindwa kutimiza ahadi yake.
Ronaldo amehuzunishwa kujikuta kuwa yupo nje ya listi ya wachezaji watatu nyota duniani wanaopata mishahara mikubwa.
Mwanasoka huyo bora wa dunia mara tano, anapata kiasi cha pauni milioni 19 kwa mwaka tofauti na makubaliano yake.
Kufuatia hali hiyo, nyota huyo ameuambia uongozi wa Real Madrid anataka kuondoka mwishoni mwa msimu huu. Hata hivyo, mreno huyo msimu huu amekuwa na kiwango kibovu, ambapo amefunga mabao manne tu.