Mwenyekti wa Bodi ya Parole nchini, Agustino Lyatonga Mrema amesema anaenda kufungua kesi ya madai baada ya watu kumzushia kifo hapo jana.
Mrema amesema watu hao wamemletea tatizo kubwa sana la kushtua familia yake na watu wake wa karibu, hivyo anaelekea TCRA ili aweze kusaidiwa kuwabaini, na kuwapeleka polisi kuwafungulia kesi.
“Walivyotangaza jana Mrema amefariki kwanza nasikitika sana, kumtangazia mtu amekufa ni kweli nilihangaika jana, mke wangu alihangaika sana, watoto wangu, marafiki zangu wapenzi wangu walikuwa wanalia kwenye simu kufuatilia hizo habari kumbe ni uzushi, ni uongo habari za kijinga kabisa, nikitoka hapa sasa hivi naenda TCRA”, amesema Mrema
Mrema ameendelea kwa kusema ..”Nitakuwa kiongozi wa kwanza katika nchi hii kuchukua hatua kali, wanipe fidia inayostahili kwa kuniletea ujinga, nataka kujua huyu mtu aliyeanzisha huu uvumi na kuweka kwenye mitandao kwa ajili ya kunifedhehesha na kuniabisha, bilioni 20 wanilipe kwa usumbufu kwa aibu niliyopata jana”.
Kwa upande mwengine Mrema amesema kitendo hiko kilimsaidia kujua ni watu gani wanampenda kweli na kina nani hawampendi, kutokana na reaction zao baada ya taarifa feki za kifo chake.