Mamlaka ya mawasiliano Tanzania, TCRA, imekipiga faini kituo cha runinga cha Star TV ya jumla ya shilingi milioni 7.5 kwa makosa ya ukiukwaji wa taratibu za kutangaza taarifa ya habari, inayotakiwa kulipwa ndani ya siku 30 kuanzia leo.
Pia mamlaka hiyo imekiweka kituo hicho cha runinga kwenye uangalizi maalum kwa muda wa miezi sita kuanzia leo kutokana na kurusha taarifa ya habari inayotajwa kuwa ya uchochezi.
Pia imekiadhibu kituo cha runinga cha Azam 2, kwa makosa ya kukiuka maadili ya uandishi wa habari na kurusha habari zenye uchochezi kuhusu uchaguzi wa madiwani.
Vituo vingine vilivyokumbwa na adhabu hiyo ni East Africa TV, Chanel Ten na ITV baada ya kuripoti habari za uchochezi.
Adhabu hizo zimetolewa leo na Mamlaka hiyo mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Akifafanua adhabu hizo leo Januari 2, 2018. Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya TCRA, Joseph Mapunda amesema Vyombo vyote vya habari vilipewa nafasi ya kutoa utetezi wao kuhusu taarifa hizo walizotoa kabla ya Mamlaka hiyo kutoa adhabu leo.
Makosa yote yaliyovikumba vituo hivyo vya Runinga ni matatu ambayo ni Uchochezi, Kukiuka maadili ya uandishi wa habari na Habari zao kukosa mizania.