Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kupitia Mkurugenzi wake, Ramadhani Kailima wameshangazwa na viongozi wa Chadema wanaosema hawatambui uteuzi wa Joseph David Njumbe kuwa mgombea wa ubunge jimbo la Singida Kaskazini.
Ramadhan Kailima ameeleza kuwa Chadema kupitia Katibu wa Wilaya wa Singida Vijijini wamekamilisha mchakato wa utambulisho wa mgombea wa Ubunge jimbo la Singida Kaskazini, Joseph Njumbe.
Ambapo Halmashauri ya Wilaya Singida iliteua wagombea 6 mmojawapo akiwa Joseph Njumbe wa Chadema, baada ya kuona amekidhi sheria, kanuni na vigezo vya katiba na chama chake cha Demokrasi na maendeleo (Chadema).
Hata hivyo Njumbe, aliwasilisha barua yake ya utambulisho iliyosainiwa na katibu wa Chadema wa Wilaya ya Singida Vijijini, Amani Mloya.
Aidha, Kailima ameeleza kuwa Joseph Njumbe, pamoja na kuwa ameshakamilisha taratibu za kupitishwa kuwa mgombea wa ubunge kwa tiketi ya CHADEMA, bado ana haki ya kikatiba ya kujiondoa katika kinyang’anyiro hicho pale tu atakapotimiza taratibu zinazotakiwa ili kujiondoa.
CHADEMA pamoja na vyama vingine vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) vilitangaza kutokushiriki uchaguzi huo mdogo wa wabunge na madiwani unaotarajiwa kufanyika Januari 18, 2018 ikidai kuwa mwenendo wa hali ya kisiasa nchini siyo shwari na kuitaka Tume ya uchaguzi kuahirisha uchaguzi huo.