Mwanachama mpya wa CCM, Alberto Msando amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Magufuli kwa kumuamini katika uteuzi wake.
Msando ambaye ni mwanamsheria amesema anaamini nafasi hiyo aliyoteuliwa na Rais Magufuli ataifanya kwa weledi ili kufanikisha malengo ya Chama cha Mapinduzi.
Kupitia akaunti yake Instagram Msando ameandika “Namshukuru Mh. Dkt. John Pombe Magufuli, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uteuzi wa kuwa Mjumbe wa Tume ya Kufuatilia Mali za Chama. Chini ya uenyekiti wa Dkt. Bashiru Ally Kakurwa na wajumbe wengine wa Tume naamini kwa dhati kazi hii itafanyika kwa weledi ili kukiwezesha chama cha Mapinduzi kujitegemea kupitia mali zake. Nawashukuru wote kwa salamu za pongezi ila kikubwa ni ushirikiano wenu kuhakikisha Tume inafanikiwa kwenye majukumu yake.“
Rais Magufuli ameteuwa timu ya watu 9 akiwemo Msando ambao wataunda tume ya kufuatilia na kuhakiki mali za CCM nchi nzima.