Mkutano mkuu wa Taifa wa Chama cha Mapinduzi nchini unaanza leo mjini Dodoma ukiwa na lengo la kumchagua Mwenyekiti wa Chama na Makamu wake wawili kutoka Tanzania bara na Zanzibar.
Chama hicho kinaendeleza mkakati wa kurejesha hadhi yake baada ya kishindo cha uchaguzi wa mwaka 2015.
Licha ya kushinda urais kwa tabu, wapinzani chini ya mwamvuli wa UKAWA walipata karibu theluthi moja ya viti vyote vya ubunge na kudhibiti halmashauri katika miji muhimu ikiwemo Dar es Salaam, hii ikiwa ni rekodi mpya.
Miaka miwili ndani ya utawala wa Rais Magufuli, upepo unaonekana kugeuka. Upinzani unaelekea kudhoofika, wakati CCM ikiimarika.
Katika siku za hivi karibuni madiwani na wabunge wa upinzani wameshuhudiwa wakihama vyama vyao kwa madai kuwa Rais Magufuli anafanya kazi nzuri.