Shughuli ya kuwaaga wanajeshi 14 wa Tanzania waliouawa wakati wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya imefanyika leo jijini Dar es Salaam.
Wanajeshi hao waliuawa baada ya kuvamiwa na waasi kwa muda wa saa 13 kufuatia waasi hao kuishambulia kambi yao nchini humo.
Sherehe hizo zimefanyika kwenye makao makuu ya jeshi la ulinzi na usalama Tanzania “Ngome” maeneo ya upanga jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa ulinzi wa amani wa Umoja wa mataifa Jean Piare Lacroix, alihudhuria sherehe hizo. Familia za wanajeshi hao nazo zilikuwepo na zimeungana na wapendwa wao kuelekea mikoani.
Shambulio hilo lilitekelezwa Alhamisi jioni kwenye kambi ya jeshi ya Semuliki eneo la Beni katika mkoa wa Kivu Kaskazini.
Taarifa ya Umoja wa Mataifa ilisema wanajeshi 5 wa jeshi la DR Congo (FARDC) waliuawa pia kwenye shambulio hilo.
Umoja wa Mataifa umesema waasi wa ADF ndio wanaotuhumiwa kutekeleza shambulio hilo lililouwa wanajeshi wengi wa Tanzania.