Mchezaji wa Misri, Mohamed Salah ameshinda Tuzo ya BBC kwa Mwanasoka bora wa Afrika Mwaka 2017.

Nyota huyu wa Liverpool alipata kura nyingi zaidi ya Pierre-Emerick Aubameyang wa Gabon, Naby Keïta wa Guinea, Sadio Mané wa Senegal na mchezaji wa Nigeria Victor Moses.

Salah, aliyefunga mabao mengi zaidi ligi kuu England, akiwa na mabao 13, amekuwa na mwaka wenye mafanikio.

Mapema 2017 alikuwa nyota wa Misri walipochukua nafasi ya pili katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika.

Baadaye mwakani, mshambuliaji huyu aliye na kasi alichangia katika magoli yote yaliyowasaidia Mafirauni kufuzu kushiriki michuano ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu 1990 – aliwasaidia wenzake kufunga mabao mawili, naye akafunga mabao matano, moja ikiwa penalti kati yao na Congo iliyowawezesha kufuzu kwa fainali hizo za Urusi.

Nchini Italia, alifunga mabao 15 na kusaidia ufungaji wa mengine 11 na kuisaidia Roma kumaliza katika nafasi ya pili kwenye Serie A, nafasi yao bora zaidi kwenye ligi katika miaka saba, kabla ya kujiunga na Liverpool na kufunga bao mara 13 katika mechi zao 16 za kwanza kwenye ligi.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *