Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa amesema wanasiasa wanaohama kutoka vyama vya upinzani kwenda CCM wanafanya uamuzi huo kutokana na uoga.

Msigwa amesema kufanya siasa ndani ya CCM kuna urahisi kuliko kufanya nje ya chama hicho kwa sababu unafanya siasa ukiwa unazungukwa na polisi na unakuwa unalindwa lakini unapokuwa upinzani unakuwa kama yatima, hali inayopelekea wengine waoga kushindwa na kuamua kwenda CCM.

Msigwa ameongeza kuwa gharama za kuwa upinzani ni kubwa ndio maana hata idadi ya wanasiasa wanaohama kutoka upinzani kwenda CCM ni wengi kuliko wanaotoka CCM kwenda upinzani na ndio maana hata baadhi ya wanasiasa hao baada ya kuona hali ya joto kisiasa imezidi kuwa kali wametangaza kurudi nyumbani CCM.

Kwa upande wa mbunge wa Temeke Abdalah Mtolea alikosoa wanasiasa wanaohama vyama na kuacha ubunge kwa kutoa sababu za kuunga mkono juhudi za Serikali.

Mtolea amesema baadhi ya wanasiasa waliotangaza kuondoka upinzani kwa kudai upinzani umeishiwa ajenda, wasichokifahamu ni kwamba vyama vya siasa haviendeshwi kwa ajenda bali vinaendeshwa kwa itikadi au misingi iliyosababisha kuundwa kwa chama cha siasa ili waweze kumaliza kero mbalimbali nchini na njia ya haraka ya kufikia maendeleo ya nchi.

Mtolea alitolea mfano tatizo la kukatika kwa umeme kuwa linaweza kuwa ajenda lakini tatizo hilo likiisha, ajenda hiyo inakua imekwisha, lakini itikadi ya chama inabaki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *