Mahakama ya juu nchini Marekani imehalalisha amri ya Rais wa nchi hiyo, Donald Trump kuzuia raia kutoka nchi sita za Kiislam kuingia chini humo.
Uamuzi huo wa Mahakama utaathiri raia wa Chad, Iran, Libya, Somalia, Syria na Yemen ambao walikuwa kwenye marufuku ya Trump.
Majaji saba kati ya tisa waliokuwa wanasikiliza shauri la pingamizi la amri hiyo waliihalalisha huku wawili wakikubaliana na pingamizi.
Hata hivyo, mahakama nyingine za San Francisco, California, Richmond na Virginia zinaendelea kusikiliza mashauri kama hayo lakini uamuzi wake utawasilishwa tena kwenye Mahakama ya Juu.
Wachambuzi wa masuala ya kisheria wameeleza kuwa kutokana na uamuzi huo wa mahakama ya juu, kuna uewezekano mkubwa kuwa mahakama nyingine zitaipa nafasi zaidi Serikali.
Rais Trump alitoa zuio hilo muda mfupi baada ya kuanza kazi ikiwa ni sehemu ya ahadi zake wakati wa kampeni, akidai ni sehemu ya mkakati wake wa kupambana na ugaidi.
Alisema atatoa utaratibu mwingine maalum wa kuwawezesha raia wema kutoka nchi hizo kuweza kuingia Marekani.