Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassimu Majaliwa amesema kuna haja ya kuangalia upya mfumo wa elimu ya juu nchini.

Majaliwa amesema kuwa sababu kuangalia upya mfumo huo ni kuuboresha uweze kusaidia kutayarisha haraka rasilimali watu walioelimika  zaidi, watakaoliwezesha taifa kuwa na maendeleo na kufikia uchumi wa kati,ifikapo mwaka 2025.

Waziri Mkuu, amesema huyo wakati akizungumza kwenye kilele cha mahafali ya 33 ya chuo kuu huria cha Tanzania, yaliyofanyika kwenye viwanja vya kanisa katoliki mkoani Singida

Akisisitiza, alisema uchumi wa kati na wa viwanda, hauwezi kufikiwa au kuwa endelevu pasipo kuwa na kiwango cha udahili katika elimu ya juu cha angalau asilimia 23.

Waziri mkuu huyo, amefafanua zaidi kwa kusema kuwa takwimu zinaonyesha kwamba karibu nchi zote washiriki katika jumuiya ya Afrika mashariki,ukiacha Burundi, zina viwango vya juu zaidi vya udahili katika elimu ya juu ikilinganishwa na cha Tanzania..

Majaliwa amesema kwa mujibu wa sera ya elimu na mafunzo 2014, mfumo wa elimu na mafunzo umetawaliwa na muundo wa kitaaluma wenye dhana ya kuchuja wahitimu kwa kila ngazi, ili kupata wachache wenye uwezo mkubwa katika taaluma.

Wakati huo huo,waziri mkuu Majaliwa, amesema serikali inaunga mkono azma ya wizara ya elimu, sayansi na teknolojia ya kuanzisha dawati maalum kwa ajili ya kuimarisha mfumo wa elimu huria na masafa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *