Klabu ya Everton inakaribia kumteua Sam Allardyce kuwa kocha wao mpya baada ya kutimuliwa kocha wao Ronald Koeman.
Mazungumzo kati ya klabu hiyo na meneja huyo yanaendelea vyema na yanaaminika kuwa karibu kuzaa matunda.
Hii ni licha ya taarifa Ureno kudokeza kwamba Everton wamevutiwa na meneja wa Shakhtar Donetsk Paulo Fonseca.
Meneja wa muda wa Everton David Unsworth anatarajiwa kuongoza klabu hiyo mechi yao ya nyumbani Ligi ya Premia dhidi ya West Ham leo usiku.
Lakini klabu hiyo huenda ikathibitisha Allardyce kuwa mrithi wa Ronald Koeman kabla ya mechi hiyo.
Koeman alifutwa na Everton mnamo 23 Oktoba baada ya klabu hiyo kushuka hadi nafasi ya 18 baada ya kuchapwa 5-2 na Arsenal nyumbani.
Allardyce, 63, alikuwa amejiondoa kutoka kwneye kinyang’anyiro cha kutaka kumrithi Koeman baada ya kukosa kupokea ofa kutoka kwa Everton mapema Novemba.
Lakini baada ya kwenda mechi saba – wakishinda moja pekee – chini ya Unsworth, ikiwa ni pamoja na kuchapwa 5-1 nyumbani na Atalanta na kushindwa 4-1 ugenini Southampton Jumapili, Everton walifufua mazungumzo na Allardyce wikendi.