Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) linahamisha mali zake kwenye jengo linalopaswa kubomolewa eneo la Ubungo lililo ndani ya hifadhi ya barabara.

Pilikapilika za wafanyakazi wa shirika hilo kuhamisha mali zinaendelea leo Jumanne Novemba 28,2017.

Kaimu Meneja Uhusiano wa Tanesco, Leila Muhaji amesema wanahamia katika ofisi zingine za shirika hilo zilizoko jijini Dar es Salaam.

Uongozi wa Tanesco katika taarifa kwa umma iliyotolewa jana Jumatatu Novemba 27,2017 ulisema umeanza utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli kuhusu kubomolewa jengo hilo.

Novemba 15,2017 akitokea Chato alipokwenda kwa mapumziko baada ya ziara ya Uganda, Rais Magufuli aliagiza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuweka alama ya X katika jengo lenye ofisi za Tanesco sehemu zilizo katika hifadhi ya barabara.

Tanesco imeanza kubomoa ukuta wa mbele ya jengo hilo na kuhamisha watumishi kupisha shughuli za ubomoaji kufanyika kwa usalama.

Uongozi wa shirika hilo na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) unaendelea kufanya utaratibu utakaowezesha ubomoaji wa jengo hilo la ghorofa kufanyika bila kuathiri huduma kwa wateja wa Tanesco.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *