Mrembo wa Afrika Kusini ameshinda taji la Mrembo wa Dunia (Miss Universe 2017) katika mchuano uliofanyika jana Jumapili jijini Las Vegas nchini Marekani.
Mrembo huyo ametunukiwa taji hilo ambapo pia hivi karibuni alitunukiwa shahada katika menejimenti ya biashara kwenye Chuo Kikuu cha North-West cha Afrika Kusini.
Akihojiwa wakati wa mashindano hayo, Nel-Peters ambaye ni mzaliwa wa Western Cape nchini humo, alisema kuna wakati aliwahi kutishwa kwa kushikiwa bunduki na watu ambao hakuwataja, akaongeza kwamba tukio hilo limemfanya kuwa na mpango wa kuwafundisha wanawake jinsi ya kujilinda.
Akijibu maswali zaidi, mrembo huyo alisema suala kubwa zaidi kwake linalomkera ni wanawake kulipwa asilimia 75 ya mshahara kwa kazi ileile ambapo wanaume hulipwa asilimia 100.
Washindi 13 walioingia fainali walitoka nchi za Thailand, Sri Lanka, Ghana, Hispania, Ireland, Croatia, Uingereza, Marekani, Brazil, Canada, Philippines, Venezuela na China.